Skip to main content

Posts

Showing posts from May, 2020

Uwiko wa kokoiko

Koo mwakorikoko,wiko jogoo huwika Hunadi kwa kokoiko,mnadi wa kuamka Koriko lake tamko,mawio ndo husikika Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika Koo wendako siko,kung'ang'ania kuwika Si swifa yako uwiko,sauti vunja mbarika Wasulubu Koo yako,na wiko halitotoka Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika Koo lako kokoreko,mjuzi kukokoreka Hukoreka kwa kereko,mwewe akishafika Ila hili kokoiko,si lako Koo kanyika Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika Koo mfanoo koko,kizazi unakiweka Ni tunu ya mola wako,Qahari alotukuka Keshakugawia lako,mbona hutaki ridhika? Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika E Koo swirati yako,njia iliyonyooka Pepo ikupelekako,kwenye mandhari tukuka Siri yake ni ridhiko,moyo wako kutosheka Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika Wasalamu nenda huko,kuliko waloridhika Wale waso unguliko,la inadi ya kuwika Waelewao tamko,tukufu lake rabuka Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika ©May 26 200 M.J.Mwinyi mwinyimwaphatsa@gmail.com #Anti- feminism

Unani ka huna una?

Mvuvi ahanahana,uwerevu umemwisha Pakacha haloni tena,mzigo wa kujitwisha Ahangana kila kona,samaki kiwazungusha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Kutwa ameuza sina,una hana wameisha Waliisha toka Jana,pakachale kuliosha Na wateja megandana,ka huna una pitisha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Leo kutoka mchana,Sasa jua linkwisha Ameuza kwa Amina,kiuzo cha kukopesha Afanyeni ana wana,anataka kuwalisha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Wateja kina Shaina,kupara kumewachosha Vidole vi tele hina,sangara atamwangusha Ndiposa wataka una,rahisi kumchemsha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Wavuvi woga wa kina,wavivu nyavu kurusha Huwapapatia una,madebe kuyafungasha Kisa wapo juu sana,hawenzi kujitabisha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Una hata ladha hana,sekunde kukinaisha Ni ja ng'onda hajanona,minofu kujipwatisha Hata paka akimwona,hamli anampisha Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha Ashangaa akiona,una wakimuitisha Wakimpangia vina,na taji wakamvisha ...

MCHUZI WA PWEZA

Nalianza tungo langu, kwa maswali kutatiza, Utamu moyoni mwangu,  kama nimepata viza, Nitapiga mtu rungu, ukweli atoliweza, KUMBE MCHUZI WA PWEZA, UTAMU UZIDI HAMU. Nawala sitatatiza, wala kuchoka mbioni, Maswala sitauliza, nitayajibu mwishoni, Nitapita kwenye kiza, ingawa mimi sioni, KUMBE MCHUZI WA PWEZA, UTAMU UZIDI HAMU.  Mwenyewe nitakubali, na kifua kujipiga, Hakika Mimi rejali, popote pale 'navyoga' Simi dume suruwali, nimeondoa uoga, KUMBE MCHUZI WA PWEZA, UTAMU UZIDI HAMU. Nguvu zote zi mwilini, hadi  zile za ziada Bora niwe kwa makini, niutowe ushuhuda Uridhike kwa mizani, uzito silete shida, KUMBE MCHUZI WA PWEZA, UTAMU UZIDI HAMU. Hichi kipya cha walili, watatu ufaidini, Nitaufanya ukali, asibaki mlangoni, Nyuki nile na hasali, juu wala sio chini, KUMBE MCHUZI WA PWEZA, UTAMU UZIDI HAMU  Wakufumbua fumbua, lengo lidhiirike, Watu pate yatambua, kila moja shike yake, Mi mgongo nananyua,  mwenyewe nipatoreke, KUMBE M...

BABAIKO

Bismillahi tamko, la mwanzoni Naanza langu andiko, kwa makiniNandikie babaiko, la nyoyoni Liuke lije zinduko, lenye kheri Naliona liko huko, ugenini Na huko vilevile liko, miijini Watu waendako siko, ni kwa nini? Wasoenda watumwako, kwenye kheri Ni utashi ulioko, wa mageni Au ni kupuza miko, ya zamani Ndiposa twenda kusiko, tumaini Bila kwogopa viboko, vya akheri Au tuna tamauko, kwa yakini Na mengi masikitiko, aushini Hatufiki tuendako, furahani Na wenzetu walo huko, masururi Haya yote yangawako, sikizani Kule ndu yangu uliko, niamini Mola kakuweka huko, mtihani Furaha au vituko, tabasuri Kuna kule uendako, kwa wendani Kule daima ambako,  kwakwauni Daima watu wa huko, hukwamini Huko ndiko upendwako, sijighuri Na kuna kule ambako, watamani Upendo huko hauko, ngaamini Wajikokota kokoko! Masikini Kutaka kisicho chako, wajighuri Bali kubali andiko, vitabuni Utapata kilo chako, kwa mizani Na ambacho sicho chako, ngatamani Katu hakiwi cha kwako, kwa...

Lipi Jema Nmetenda?

Kila lizamapo jua, wangu moyo ushamaka Nawaza na kuwazua, siku imetamatika Hesabu nazichambua, machozi yakinitoka Lipi jema nimetenda, kumridhisha Jalia? Maswali bila majibu, kichwani yanajijaza Wapi nilipoharibu, na wapi nimetengeza Peke yangu kama bubu, nabaki kujisemeza Lipi jema  nimetenda, kumridhisha Manani?* Siku imeshanipita, kama maji kwenye mawe Riziki nikitafuta, kaniruzuku mjawe Nafusi inanisuta, yauliza 'vipi wewe'? Lipi jema nimetenda, kumridhisha Karima? Hatua nizipigapo, siachi kufikiria Mfano hapa nilipo, roho ikinikimbia Je nitaipata pepo?, hapo ndipo nakwamia Lipi jema nimetenda, kumridhisha Mwenyezi? Katu hazihesabiki, anazonipa neema Kwenye fungu la riziki, daima siachwi nyuma Moyo unanishitaki, hauachi kunisema Lipi jema nimetenda, kumridhisha Muumba? Kanilinda na majanga, kwa mbali yanipitia Kaniepusha na wanga, wasiwahi nifikia Duniani ninaringa, je yeye afurahia? Lipi jema nimetenda, kumridhisha Qudusi? Meingia mtukufu, mw...

Lost in my own world.

Do you often find yourself off mood and thinking of things that are out of your control. It happens to me so often, and when it does, it crumbles the little spirit and strength I have to stand up and show up every other time am needed. Needless to say , I fall victim of my expectations and the experiences I have had to live, again thinking of what went wrong and how many times I failed myself in all what I thought I would accomplish. It’s a hard experience thinking about it, because in the outside you are kinda okay and energised but deep down you are oozing blood profusely. It’s typical for people to say, accept the decree of God, but that sounds like a cliché to me , don’t confuse me for not being a believer, I accept the Decree of God and adhere to it religiously, it’s only that this feeling sweeps you off your feet and gets you thinking, what if ? In the end , you become a wrecked ship. I rarely share this feeling out, it’s like I am okay and yet I am not okay. So today I got t...

MAMA NI MAMA

Bismillah Raufu, Mola aliyetukuka, Sinalo la kukashifu, kasema litaumbuka, Leo hai kesho mfu, katuumba Yah Rabuka, Naitafuta zawadi, niweze mlipa mama,  Tatu haki mama twaa, nne yake yeye baba, Nipate nuru ya taa, laana ndio msiba, Mama naomba nufaa, nisijidunge na mwiba, Naitafuta zawadi, niweze mlipa mama Kila kona natafuta, lakini sijaona, Machozi yangu nafuta, namuomba Rabana, Sitaki mie kujuta, nikaikosa jahana, Naitafuta zawadi, niweze mlipa mama  Nashukuru ni mzima, afia nguvu anazo, Aniiti kunituma, wala sinao mzozo, Namtendea mema, kwake sina ya likizo, Naitafuta zawadi, niweze mlipa mama  Mama leo samahani, hadharani nayasema, Sipo kuona machoni, baridi wangu mtima, Ila furaha moyoni,nakupenda sana mama. Naitafuta zawadi,niweze mlipa mama. By Wiseman Abubakar +254783101884

TUSIMDHARAU MAMA

Ni furaha tele tele,pamoja tushangilie Walipo popote pale,shangwe mama asikie Sherehe pamoja tule,siku yao 'furahie Tusimdharau mama! Insi wote duniani,wote katoka kwa mama Miezi tisa jamani,alivumilia mama Tangu wetu utotoni,katulea sote vyema Tusimdharau mama! Mwalimu wa kwanza mama,yote mema kafundisha Hakuchoka katu mama,penzi lake kazidisha Mambo yote yale mema,katia sana puresha Tusimdharau mama! Na aliye kama mama,Mikaeli sijamwona Hakika hakati tama,hamtelekezi mwana Kinagaga nasema,mama ni kama Rabana Tusimdharau mama! Beti tano nikitua,nakuomba tafadhali Furusa hii chukua,mzawadi tafadhali Atakuombea dua,baraka zake Jalali Tusimdharau mama! MTUNZI: MICHAEL COSMAS +254751388636 michaelcosmas96@gmail.com

Shukrani Kina Mama.

Hisani ya pixabay.com Semi mdomo husemi,leo kalamu yatema, Wala haina ugomi,leo mama kumsema, Kweli siku haziyemi,miaka imeandama, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea, Kweli maana ya mama, waijuao wenyewe, Kamusini tutasoma,bado tusiwaelewe, Tujaribu kutazama,vitendo vyao twelewe, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea, Yaini tulidondoka,bada miezi tisia, Vifaranga ndo kufika,duniani twaingia, Hatujui kujiruka,kwenu tulijifunzia, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea Kufoka 'litufokea,hilo hatuwezi pinga, Mateke yakatembea,miili mkairanga, Tulihisi 'tuonea, ila ndo mlitujenga, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea. Kwa kucha mlichakura,kutwa tuyapate lishe, Kazi bila mshahara,'liziita mishe mishe, Japo ni kwa mutura,'lihustle mtulishe, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea. Baridi hatukufili,mama mkiwa jawabu, Joto lisilo mithili,nyie ndo mkawa blabu, Malezi yalo kamili,mlitupa bila jibu, Shukrani kina mama,vifaranga kutulea. Mgongoni tigat...

CLOAKED

Photo courtesy pixabay.com  Love. The automatic thought when the heart is mentioned. Unless you are studying the organ in class or dissecting its parts in a laboratory, pumping blood will not be what floats to your oblongata. Unless you have Obsessive Compulsive Disorder. Or belong to the crowd where rigidity is the way to live. So much so is the association that one claiming heart is their favourite symbol will be linked automatically to being loving and likeable and friendly. Hate. The direct and opposite reaction to love. There is no shape for it. It must feel lonely every so often. Its mention only coming in the bad times. Abandoned when things are flowing smoothly. Substituted when love fails and hope cannot be restored. Used as a mere replacement when alternate feelings cease to align. Some represent it using the middle finger. Some lash out with cuss words. The best representative one can find for hate is the cross sign which reads more of dislike. Even people who ...

MHIMILI YA FURAHA.

Picha hisani ya pixabay.com  Bismillahi Jalali, mtunzi natangulia Nina ujumbe wa kweli, nataka kuwaambia Yatege yote mawili, upate kunisikia   Ili uwe na furaha, kwa Muumba tawakali Ukisha kutawakali, Mola kumtegemea Kuna suala la pili, nataka kukuambia Yapasa ujikubali, haliyo ya kidunia   Ili uwe na furaha, ndugu yangu jikubali Na ukisha jikubali, usikae kutulia Mola kakupa akili, hebu sasa itumia Utende lile na hili, jema lolifikiria   Ili uwe na furaha, ndu yangu jipe shughuli Siwe mtu usojali, baradhuli dontkea Kiwavya utawa nduli, wenzako kukuchukia Kikanywa wawa mkali, kinywa wazi wakemea   Ili uwe na furaha, siwe mtu usojali Bali sawa ya khiswali, maisha kukupambia Uwe mwenye kukubali, aso unapokosea Hadhi yako kuijali, na za wengineo pia   Ili uwe na furaha, jijali na utujali Ukisema sema kweli, kauli ukitongoa Ukitenda tenda kweli, tendo jema wafikia Sifayo iwe ukweli, kiwa hujui tulia   Ili uwe na furaha, se...

SIMU KWA MHESHIMIWA GAVANA

Hello hello shika simu, Mkubwa nakupigia, Napiga nazo nidhamu, naomba kunisikia, Zangu salamu muhimu, nataka kukuambia, Mheshimiwa gavana, ujumbe huu ni wako, Ujumbe huu ni wako, mwaphombo nasimulia, Nayanena  yalioko, uchungu tena nalia, Wadogo wako vicheko, na wanyonge waumia, Mheshimiwa gavana, uzalendo wapotea, Uzalendo wapotea, kwa unyanyaso kuzidi, Wapo waliopotea, kwa ukaidi kuzidi, Uovu waendelea, masikini hafaidi, Mheshimiwa Gavana, tamaa bado wanazo, Tamaa bado wanazo, wakiwa maofisini, Kwetu huleta mzozo, wangali wamo kazini, Huleta na matatizo, walala hoi  wa chini, Mheshimiwa Gavana, timu yako yakuponza, Timu yako yakuponza, hizo kazi unawapa, Wakimbia wao kwanza, wachochole kuwachupa, Lipi sasa watufunza,  kama wao waliapa, Mheshimiwa Gavana, wapatia masharuti, wapatia masharuti, wazingatie kindani, Yalipitwa na wakati,  zamani za ukoloni, Wafanye ya hairati, kuweka yao mizani, Mheshimiwa Gavana, sifazo wasiboronge Sifazo wasibo...