Koo mwakorikoko,wiko jogoo huwika
Hunadi kwa kokoiko,mnadi wa kuamka
Koriko lake tamko,mawio ndo husikika
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
Koo wendako siko,kung'ang'ania kuwika
Si swifa yako uwiko,sauti vunja mbarika
Wasulubu Koo yako,na wiko halitotoka
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
Koo lako kokoreko,mjuzi kukokoreka
Hukoreka kwa kereko,mwewe akishafika
Ila hili kokoiko,si lako Koo kanyika
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
Koo mfanoo koko,kizazi unakiweka
Ni tunu ya mola wako,Qahari alotukuka
Keshakugawia lako,mbona hutaki ridhika?
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
E Koo swirati yako,njia iliyonyooka
Pepo ikupelekako,kwenye mandhari tukuka
Siri yake ni ridhiko,moyo wako kutosheka
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
Wasalamu nenda huko,kuliko waloridhika
Wale waso unguliko,la inadi ya kuwika
Waelewao tamko,tukufu lake rabuka
Uwiko wa kokoiko,Koo si wako bazika
©May 26 200 M.J.Mwinyi
mwinyimwaphatsa@gmail.com
#Anti- feminism

Comments
Post a Comment