Bismillahi Jalali, mtunzi natangulia
Nina ujumbe wa kweli, nataka kuwaambia
Yatege yote mawili, upate kunisikia
Ili uwe na furaha, kwa Muumba tawakali
Ukisha kutawakali, Mola kumtegemea
Kuna suala la pili, nataka kukuambia
Yapasa ujikubali, haliyo ya kidunia
Ili uwe na furaha, ndugu yangu jikubali
Na ukisha jikubali, usikae kutulia
Mola kakupa akili, hebu sasa itumia
Utende lile na hili, jema lolifikiria
Ili uwe na furaha, ndu yangu jipe shughuli
Siwe mtu usojali, baradhuli dontkea
Kiwavya utawa nduli, wenzako kukuchukia
Kikanywa wawa mkali, kinywa wazi wakemea
Ili uwe na furaha, siwe mtu usojali
Bali sawa ya khiswali, maisha kukupambia
Uwe mwenye kukubali, aso unapokosea
Hadhi yako kuijali, na za wengineo pia
Ili uwe na furaha, jijali na utujali
Ukisema sema kweli, kauli ukitongoa
Ukitenda tenda kweli, tendo jema wafikia
Sifayo iwe ukweli, kiwa hujui tulia
Ili uwe na furaha, sema na tenda ya kweli
Kisha tupilia mbali, mambo yalotangulia
Moyo usiwe hamali, wa kero za kidunia
Yalotendeka azali, hayawezi jirudia
Ili uwe na furaha, moyoo siwe hamali
Moyoo siwe hamali, madhambi kajibebesha
Sitamauke kwa hili, kajihukumu mekwisha
Tubu toba ya kikweli, toba itakusafisha
Ili uwe na furaha, siache istighfari
Sijerefusha kauli, kheri ikawa udhia
Ingawa tamu asali, husinya ikizidia
Naondoka msijali, kwaheri nawaambia
Ungaitaka furaha, hiyo ndiyo mihimili
Mwaphatsa Suleiman,
Mneni Moyoni,
Abuu Hulaimah.

Comments
Post a Comment