Kila lizamapo jua, wangu moyo ushamaka
Nawaza na kuwazua, siku imetamatika
Hesabu nazichambua, machozi yakinitoka
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Jalia?
Maswali bila majibu, kichwani yanajijaza
Wapi nilipoharibu, na wapi nimetengeza
Peke yangu kama bubu, nabaki kujisemeza
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Manani?*
Siku imeshanipita, kama maji kwenye mawe
Riziki nikitafuta, kaniruzuku mjawe
Nafusi inanisuta, yauliza 'vipi wewe'?
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Karima?
Hatua nizipigapo, siachi kufikiria
Mfano hapa nilipo, roho ikinikimbia
Je nitaipata pepo?, hapo ndipo nakwamia
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Mwenyezi?
Katu hazihesabiki, anazonipa neema
Kwenye fungu la riziki, daima siachwi nyuma
Moyo unanishitaki, hauachi kunisema
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Muumba?
Kanilinda na majanga, kwa mbali yanipitia
Kaniepusha na wanga, wasiwahi nifikia
Duniani ninaringa, je yeye afurahia?
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Qudusi?
Meingia mtukufu, mwezi mwema Ramadhwani
Hajanifanya kipofu, meshuhudia machoni
Siwezi lipa sarafu, manoti wala mapeni
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Raufu?
Refu lisilo na mwisho, sijawahi kusikia
Hapa ndio hitimisho, Manyota namalizia
Si leo wala si kesho, swali linajirudia
Lipi jema nimetenda, kumridhisha Rabbana?
Nassoro Abu
Manyotta Malenga Mtanashati
©002 Waa
Comments
Post a Comment