Hello hello shika simu, Mkubwa nakupigia,
Napiga nazo nidhamu, naomba kunisikia,
Zangu salamu muhimu, nataka kukuambia,
Mheshimiwa gavana, ujumbe huu ni wako,
Ujumbe huu ni wako, mwaphombo nasimulia,
Nayanena yalioko, uchungu tena nalia,
Wadogo wako vicheko, na wanyonge waumia,
Mheshimiwa gavana, uzalendo wapotea,
Uzalendo wapotea, kwa unyanyaso kuzidi,
Wapo waliopotea, kwa ukaidi kuzidi,
Uovu waendelea, masikini hafaidi,
Mheshimiwa Gavana, tamaa bado wanazo,
Tamaa bado wanazo, wakiwa maofisini,
Kwetu huleta mzozo, wangali wamo kazini,
Huleta na matatizo, walala hoi wa chini,
Mheshimiwa Gavana, timu yako yakuponza,
Timu yako yakuponza, hizo kazi unawapa,
Wakimbia wao kwanza, wachochole kuwachupa,
Lipi sasa watufunza, kama wao waliapa,
Mheshimiwa Gavana, wapatia masharuti,
wapatia masharuti, wazingatie kindani,
Yalipitwa na wakati, zamani za ukoloni,
Wafanye ya hairati, kuweka yao mizani,
Mheshimiwa Gavana, sifazo wasiboronge
Sifazo wasiboronge, twaona na atusemi,
Tena ofisi wachunge, uwakatishe ulimi,
Na pabaya uvurunge, wafate wako mfumi,
Mheshimiwa Gavana, Kwale bado twaipenda
Kwale bado twaipenda, wallah billah tena,
Umoja si kuuvunda, kwa maneno ya fitina,
Na mema nikuyapanda, tuyasahau ya jana,
Mheshimiwa Gavana, utofauti tuwache,
Utofauti tuwache, maendeleo tufanye,
Pa kombo usipafiche, wala sio kupapenye
Na mabahili wachache, ni vyema si tuwakanye,
Mheshimiwa Gavana, jasho lako twalijua,
Hapa mwisho nimefika, simu yangu naikata,
Nisameheni hakika, iwapo mevuka kuta,
KWALE NI KUBADILIKA, TUONDOWENI UTATA
Mheshimiwa Gavana, hongera kwa kazi yako
Wiseman Abubakar
Maganya
_002
_Thank you B.M.Y.G_
Comments
Post a Comment