Bismillahi tamko, la mwanzoni
Naanza langu andiko, kwa makiniNandikie babaiko, la nyoyoni
Liuke lije zinduko, lenye kheri
Naliona liko huko, ugenini
Na huko vilevile liko, miijini
Watu waendako siko, ni kwa nini?
Wasoenda watumwako, kwenye kheri
Ni utashi ulioko, wa mageni
Au ni kupuza miko, ya zamani
Ndiposa twenda kusiko, tumaini
Bila kwogopa viboko, vya akheri
Au tuna tamauko, kwa yakini
Na mengi masikitiko, aushini
Hatufiki tuendako, furahani
Na wenzetu walo huko, masururi
Haya yote yangawako, sikizani
Kule ndu yangu uliko, niamini
Mola kakuweka huko, mtihani
Furaha au vituko, tabasuri
Kuna kule uendako, kwa wendani
Kule daima ambako, kwakwauni
Daima watu wa huko, hukwamini
Huko ndiko upendwako, sijighuri
Na kuna kule ambako, watamani
Upendo huko hauko, ngaamini
Wajikokota kokoko! Masikini
Kutaka kisicho chako, wajighuri
Bali kubali andiko, vitabuni
Utapata kilo chako, kwa mizani
Na ambacho sicho chako, ngatamani
Katu hakiwi cha kwako, kwa qadari
Ni ukingoni niliko, Sulemani
Tuliwache sikitiko, ikhiwani
Huko ndu zangu tuliko, shukuruni
Na kama kuna vituko, tusubiri
Mwaphatsa Suleiman,
Mneni Moyoni,
Abuu Hulaimah.
Comments
Post a Comment