Mvuvi ahanahana,uwerevu umemwisha
Pakacha haloni tena,mzigo wa kujitwisha
Ahangana kila kona,samaki kiwazungusha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Kutwa ameuza sina,una hana wameisha
Waliisha toka Jana,pakachale kuliosha
Na wateja megandana,ka huna una pitisha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Leo kutoka mchana,Sasa jua linkwisha
Ameuza kwa Amina,kiuzo cha kukopesha
Afanyeni ana wana,anataka kuwalisha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Wateja kina Shaina,kupara kumewachosha
Vidole vi tele hina,sangara atamwangusha
Ndiposa wataka una,rahisi kumchemsha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Wavuvi woga wa kina,wavivu nyavu kurusha
Huwapapatia una,madebe kuyafungasha
Kisa wapo juu sana,hawenzi kujitabisha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Una hata ladha hana,sekunde kukinaisha
Ni ja ng'onda hajanona,minofu kujipwatisha
Hata paka akimwona,hamli anampisha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Ashangaa akiona,una wakimuitisha
Wakimpangia vina,na taji wakamvisha
Ladha hana nyama hana,ila mbawa kajivisha
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
Nauliza waungwana,swali kwenu nalirusha
Kwanini mwapenda una,samaki asoridhisha?
Ni kwamba magamba hana,au bei ya kurusha?
Unani ka huna una?ndo swali lilomchosha
©M.J.Mwinyi,30th May 2020
mwinyimwaphatsa@gmail.com

Comments
Post a Comment