Skip to main content

Posts

Showing posts from April, 2020

MBAYUMBAYU.

Kinda leo nimekuwa, umri natinga makamo, Wazo ndoa meamuwa,kufuata waliomo, Ila miti yazinguwa,kutua wa kipi kimo, Mbayuwayu ninatanga,mti gani niutue. Mchungwa wa ngombeni,kuutua abadani, Miba mvungururini,itanidunga mwilini, Mwanzo uko taabani,kukaukia nyumbani, Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue. Mkorosho wa denyenye,kuutua sitamani, Unapendwa na bwanyenye,ataukata shinani, Ndoto zangu zitawanye,aniwache mataani, Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue. Mchenza pale kombani,kuutua nina shaka, Tunda rangi kijani,machoni utalitaka, Ila sinao imani,utaoza kwa haraka, Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue. Mnazi wa hapo vuga,kuutua ni mikosi Mwenzenu utaniyuga,msiri kama kamisi, Utanishinda kuparaga,una miba ya matusi, Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue. Mkunazi wa vyongwani,maarufu hapo tsimba, Wapuraji mawe teni,naogopa ana mimba, Wengi watajamuwini,anahongeka mshamba, Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue. Mbambakofi wa jeza, kutuua ni balaa, Masharti ...

Wanafunzi Warandaranda.

Jamani tufanye nini, watoto wawe nyumbani? Yani nikiwa garini, ninawaona njiani, Hawana hofu nyoyoni, na janga la duniani, Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui. Vinara maofisini, na vijakazi wa chini, Wote wamo baitini, Korona wakimbieni, Ila watoto jamani, wanaranda mitaani, Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui. Mewasikia yakini, kisema tukachezeni, Wajitia hatarini, wangiapo viwanjani, Mana hakuna sabuni, na wagusana nyusoni, Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui. Aloathirika nani, mzima hajulikani, Pamoja twawaonani, wakitembea kundini, Umbali hawatengani, ilivyowekwa kanuni, Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui. Nina wazo akilini, vijana tujipangeni, Tuingie mitaani, na viboko mikononi, Kichapo tutembezeni, kwa kila aso nyumbani, Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui. Sitawa sana mneni, ninatinga kikomoni, Wazazi nawambieni, watoto tuwakanyeni, Mana virusi njiani, watavileta chengoni, Wazuwieni nyumbani, hadi Korona iishe. Mtoto wa Madam ...

Waridi

Waridi ni ua zuri, lenye harufu murua Waridi kama ambari, si kokote huchanua Waridi lataka ari, ya kwenda kulichukua Waridi ua la shani Waridi lataka tunzwa, kwa matunzo mbali mbali Waridi si la kupuzwa, na kutupiliwa mbali Waridi ni kama kichwa, ni muhimu kwenye mwili Waridi ua la shani Waridi silikanyage, mpaka likachanika Waridi usilisage, haibaye ikatoka Waridi sio lirege, thamaniye ikashuka Waridi ua la shani Waridi liengeenge, ulibebe kama yai Waridi usilisonge, ukalitoa hai Waridi vyema lipange, pia ulirairai Waridi ua la shani Waridi 'mepeleleza, mpaka nikamaizi Waridi ukilitunza, na sana ukilienzi Waridi litapendeza, na lingae kama mwezi Waridi ua la shani ashikiwakiswahili Farwat Sharif

Chapati Zikiwa ngumu.

Chapati zikiwa ngumu, kiwango cha kutolika Hazitamu hazinyamu, na kooni kutoshuka Nani wa kumlaumu, nipe jibu la hakika Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu Au tunaweza sema, ni yule wa kiwandani Kazi haijui vyema, na wala hana makini Na hawezi kujituma, kufanya unga laini Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu Pengine ni mkandaji, hajui vyema kupika Hanacho yeye kipaji, kukanda ukakandika Au hafahamu maji, ya kwenye unga kuweka Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu Au labda ni samli, hakujua kukisia 'Litia bila kujali, kiwango mahususia Labda hapo ndo kafeli, shaghala kujikandia Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu Au mwenye kusukuma, pengine amechangia Hakuzisukuma vyema, nene aliziachia Au mwasemaje jama, akilini laingia? Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu  Pengine alozipika, hakuwa nayo makini Alikuwa na haraka, ya kuwahi kipindini 'Mekuwa ngumu hakika, haziliki abadani Chapati zikiwa ngumu,ni nani tumlaumu ashikiwakiswahili Farwat...