Chapati zikiwa ngumu, kiwango cha kutolika
Hazitamu hazinyamu, na kooni kutoshuka
Nani wa kumlaumu, nipe jibu la hakika
Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu
Au tunaweza sema, ni yule wa kiwandani
Kazi haijui vyema, na wala hana makini
Na hawezi kujituma, kufanya unga laini
Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu
Pengine ni mkandaji, hajui vyema kupika
Hanacho yeye kipaji, kukanda ukakandika
Au hafahamu maji, ya kwenye unga kuweka
Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu
Au labda ni samli, hakujua kukisia
'Litia bila kujali, kiwango mahususia
Labda hapo ndo kafeli, shaghala kujikandia
Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu
Au mwenye kusukuma, pengine amechangia
Hakuzisukuma vyema, nene aliziachia
Au mwasemaje jama, akilini laingia?
Chapati zikiwa ngumu, ni nani tumlaumu
Pengine alozipika, hakuwa nayo makini
Alikuwa na haraka, ya kuwahi kipindini
'Mekuwa ngumu hakika, haziliki abadani
Chapati zikiwa ngumu,ni nani tumlaumu
ashikiwakiswahili
Farwat Sharif

Comments
Post a Comment