Kinda leo nimekuwa, umri natinga makamo,
Wazo ndoa meamuwa,kufuata waliomo,
Ila miti yazinguwa,kutua wa kipi kimo,
Mbayuwayu ninatanga,mti gani niutue.
Mchungwa wa ngombeni,kuutua abadani,
Miba mvungururini,itanidunga mwilini,
Mwanzo uko taabani,kukaukia nyumbani,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mkorosho wa denyenye,kuutua sitamani,
Unapendwa na bwanyenye,ataukata shinani,
Ndoto zangu zitawanye,aniwache mataani,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mchenza pale kombani,kuutua nina shaka,
Tunda rangi kijani,machoni utalitaka,
Ila sinao imani,utaoza kwa haraka,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mnazi wa hapo vuga,kuutua ni mikosi
Mwenzenu utaniyuga,msiri kama kamisi,
Utanishinda kuparaga,una miba ya matusi,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mkunazi wa vyongwani,maarufu hapo tsimba,
Wapuraji mawe teni,naogopa ana mimba,
Wengi watajamuwini,anahongeka mshamba,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mbambakofi wa jeza, kutuua ni balaa,
Masharti sitoyaweza,sitopata furahaa,
Watengeneza jeneza,kunizikia shujaa,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mkungu ulo kinango,kuutua ni simanzi,
Siupendi kimpango,tangia za babu enzi,
Kunguze zina ukongo,utanitia majonzi,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mkakasi wa ndavaya,kuutua ni muhali,
Kimo chake tanipwaya,juu mekwenda mbali,
Na wake huo ubaya, wamea kila mahali,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mgomba wa tiwi digo,kutua shida kwa kinda,
Mkungu wake mzigo,na ndugu waliopinda,
Mazao yake kidogo, kigogo utanishinda,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mvinde hapo ukunda, tanizidi maarifa
Kuumiliki tadinda,kumea kwake masafa,
Na sherehe za kushinda,mfukoni ni maafa,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mkoma wa msambweni,kuutua sio shangwe,
Koma zake za kihuni,nyumbani tele mbwembwe,
Na vyama visandukuni,kiunoni na kibwebwe,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Minyaa mwananyamala,kuitua nina doa,
Kunimiliki mwabala,yakini hutatoboa,
Hauna nguvu ka swala,taniangusha si poa,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Mwembe wa lungalunga,kuutua niugue,
Kumwelewa majanga,ni boribo ama ngoe,
Usiku apiga dunga,mchana dua apoe,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
Sijatukana mkunga,na uzazi ungalipo,
Ila mambo kujipanga,kujikuna uwashwapo,
Yupi atajaniunga,pamoja tule kiapo,
Mbayuwayu ninatanga,kwale mji niutue.
@gwijiwamashairi
Athuman_mswahili
Comments
Post a Comment