Jamani tufanye nini, watoto wawe nyumbani?
Yani nikiwa garini, ninawaona njiani,
Hawana hofu nyoyoni, na janga la duniani,
Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui.
Vinara maofisini, na vijakazi wa chini,
Wote wamo baitini, Korona wakimbieni,
Ila watoto jamani, wanaranda mitaani,
Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui.
Mewasikia yakini, kisema tukachezeni,
Wajitia hatarini, wangiapo viwanjani,
Mana hakuna sabuni, na wagusana nyusoni,
Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui.
Aloathirika nani, mzima hajulikani,
Pamoja twawaonani, wakitembea kundini,
Umbali hawatengani, ilivyowekwa kanuni,
Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui.
Nina wazo akilini, vijana tujipangeni,
Tuingie mitaani, na viboko mikononi,
Kichapo tutembezeni, kwa kila aso nyumbani,
Walitolewa shuleni, na nyumbani hawatui.
Sitawa sana mneni, ninatinga kikomoni,
Wazazi nawambieni, watoto tuwakanyeni,
Mana virusi njiani, watavileta chengoni,
Wazuwieni nyumbani, hadi Korona iishe.
Mtoto wa Madam Riziki
Ibrahim Mohamed Yeya
ibrahimyeya@gmail.com
+254 711 393 805/+254 736 409 422
Kwale, Kenya
Comments
Post a Comment