Waridi ni ua zuri, lenye harufu murua
Waridi kama ambari, si kokote huchanua
Waridi lataka ari, ya kwenda kulichukua
Waridi ua la shani
Waridi lataka tunzwa, kwa matunzo mbali mbali
Waridi si la kupuzwa, na kutupiliwa mbali
Waridi ni kama kichwa, ni muhimu kwenye mwili
Waridi ua la shani
Waridi silikanyage, mpaka likachanika
Waridi usilisage, haibaye ikatoka
Waridi sio lirege, thamaniye ikashuka
Waridi ua la shani
Waridi liengeenge, ulibebe kama yai
Waridi usilisonge, ukalitoa hai
Waridi vyema lipange, pia ulirairai
Waridi ua la shani
Waridi 'mepeleleza, mpaka nikamaizi
Waridi ukilitunza, na sana ukilienzi
Waridi litapendeza, na lingae kama mwezi
Waridi ua la shani
ashikiwakiswahili
Farwat Sharif

Comments
Post a Comment