pixabay.com free images
Ndugu zangu nawaomba, mwenzenu 'saidieni,
Mana nishagonga mwamba, sijui nifanye nini,
Dau langu linayumba, lataka zama majini,
'Limpenda kanikana, sasa anitaka tena.
'Limpenda kanikana, sasa anitaka tena,
Na nilipata kimwana, wenyewe tunaendana,
Mtoto mzuri sana, wa kumzidi hakuna,
Ila naye ni kicheche, wengi wanamtambua.
Ila naye ni kicheche, wengi wanamtambua,
Hatembei na wachache, penzini hajatulia,
Hunichoma kama cheche, moyoni nikaumia,
Ila nataka mfunza, huenda akageuka.
Ila nataka mfunza, huenda akageuka,
Mana vyema hunitunza, hadi nikafurahika,
Na huyu mwingine mwenza, tabia 'mekamilika.
Tatizo alinigura, wakati 'lipomtaka.
Tatizo alinigura, wakati 'lipomtaka,
Ninahisi ufukara, ndo chanzo cha kunepuka,
Kwa sasa nami nang'ara, ndio kwangu achipuka,
Amekuja kuniomba, nimpe wangu mtima.
Amekuja kuniomba, nimpe wangu mtima,
Kweli ilopo ni kwamba, mamboye yote ni mema,
Janga linalonikumba, nitamwacha nani nyuma?
Mana yeye yu kamili, na huyu vyema atunza.
Mana yeye yu kamili, na huyu vyema atunza.
Wa pili ana thakili, ujauzito kuanza,
Anachukulia hili, kufanya kathiri manza,
Nyumbani hubadilisha, waume aina nyingi.
Nyumbani hubadilisha, waume aina nyingi,
Jamani yamenichosha, hapa naweka kigingi,
Mpira kwenu narusha, mulio akili nyingi,
Naombeni zenu rai, nambieni nifanyeje
Mtunzi
Mtoto wa Madam Riziki
Ibrahim Mohamed Yeya
Kwale, Kenya

Comments
Post a Comment